Utangulizi |
|
Wilaya ya Mvomero ni moja kati ya Wilaya 5 (tano) za Mkoa wa Morogoro. Wilaya hii imeanzishwa mwaka 2002 na ina jumla ya kilomita za mraba 7,325 sawa na 9.98% ya eneo la Mkoa. Wilaya ina jimbo moja la Uchaguzi wa Ubunge la Mvomero linaloanzia Mgeta kwenye Milima ya Uluguru hadi Turiani kwenye Milima ya Nguu. Wilaya inapakana na Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kwa upande wa Kaskazini na Wilaya ya Kilosa kwa upande wa Magharibi. Kwa upande wa Kusini inapakana na wilaya Morogoro na kwa upande wa Kaskazini Mashariki inapakana na wilaya za Bagamoyo na Handeni.
|
|
|
UMBILE LA ARDHI |
|
Umbile la Wilaya ni kama mwezi mchanga unaoambaa ambaa Manispaa ya Morogoro kuelekea Kaskazini. Kijiografia Wilaya imegawanyika katika nyanda tatu kama ifuatavyo:-
• Nyanda za juu ( Highland and Mountainous Zone):
Nyanda hizi hasa ni zile za milima ya Uluguru na Ungulu. Eneo hili limechukua 25% ya eneo la Wilaya. Nyanda hizi zipo kwenye mwinuko wa mita 1200 – 2000 kutoka usawa wa bahari. Nyanda hizi zinafaa kwa mazao ya biashara kama vile; kahawa, Hiliki na mazao ya chakula kama mahindi, maharage, mboga, ndizi, viungo na matunda.
• Nyanda za chini (Low and Semi Mountainous Zone):
Nyanda hizi zipio kwenye mwinuko wa mita 800 hadi 1200 kutoka usawa wa bahari. Nyanda hizi hustawisha mazao kama mahindi, mihogo, mtama kwa chakula na mazao ya biashara ni Miwa na Alizeti. • Nyanda za Tambarare (Savannah Zone):
Nyanda hizi zipo kwenye mwinuko (altitude) wa mita 600 – 800 kutoka usawa wa bahari. Mazao yanayostawi kwenye nyanda hizi ni mpunga, Mahindi, na Mihogo kama mazao ya chakula, na mazao ya biashara ni Miwa, Pamba na Katani.
|
|
|
|
IDADI YA WATU |
|
Kutokana na sensa ya mwaka 2002, Wilaya ina wakazi wapatao 260,525 kati yao wanaume ni 131,256 na wanawake 129,269. Jumla ya Kaya katika Wilaya ni 58,314 zenye wastani wa watu 4.5 kwa kila Kaya. Ongezeko la watu kwa mwaka ni 2.6%.Wilaya inaonyesha kuwa na nguvu kazi ya watu 142,755 sawa na 54.8% ya wakazi wote 260,525.
|
|
Hali ya Hewa |
Kwa kawaida Wilaya inapata mvua mara mbili kwa mwaka. Mvua za vuli, ambazo huanza mwezi Oktoba hadi Januari. Mvua za masika, ambazo huanza mwezi Februari hadi Mei/Juni. Wilaya hupata wastani wa 1900mm za mvua kwa mwaka. Hali ya joto ni nyuzi 29 0 C
|
Utawala |
Halmashauri ina jimbo moja la uchaguzi ambalo ni Mvomero na Bw Paul C. Kiyumbi ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri na Bibi S. Linuma ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
|
|
Sekta ya Kilimo |
|
Hali ya Kilimo
Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mvomero. Asilimia 84.1% ya wakazi wa Wilaya wanajishughulisha na Kilimo na ufugaji. Eneo linalofaa kwa kilimo ni Hekta 549,375 na eneo linalolimwa ni Hekta 247,219 sawa na 45% ya eneo lote linalofaa kwa kilimo. Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni Hekta 20,579 lakini eneo linalomwagiliwa ni Hekta 5,281 . Idadi ya wakulima ni 142,755 ambao kati yao wanaume ni 71,922 na wanawake ni 70,833.
|
|
Maeneo ya uzalishaji |
Katika kutekeleza mpango huu, Halmashauri iLiainisha maeneo maalumu ya kuanzia katika mpango huu kwa mwaka 2007/2008. Maeneo yamegawanywa katika Kanda tano, zenye Kata kumi na moja (11) na vijiji 44 kati ya vijiji 132 vya Wilaya ya Morogoro, Mazao yaliyohusishwa ni Mpunga, Mahindi na jamii ya mikunde.
|
|
|
Upatikanaji wa pembejeo.
|
Pembejeo zilipatikana vizuri katika maduka ya mawakala wa pembejeo walioko mjini. Pembejeo zenye ruzuku pia upatikanaji wake ulikuwa mzuri, wakulima walipata mahitaji yao kupitia mawakala.
Pembejeo za ruzuku zilizopatikana ni mbolea aina ya urea tani 76, DAP tani 20 na mbegu za mahindi 2.2. Ambazo zilinunuliwa na mawakala na kuuzwa kwa wakulima. Wakulima walipata pembejeo kupitia mawakala waliopo vijijini na mjini.Vile vile wakulima katika vijiji 15 vya wilaya waliweza kuzalisha mbegu bora za mahindi tani 10 na kuwauzia wakulima wenzao kwa bei nafuu .Hii iliwezekana baada kupata mafunzo ya kuzalisha mbegu bora chini ya mradi wa ASDP.
|
|
Ushirika na Masoko |
|
Hali ya Ushirika:
Shughuli za Ushirika katika Wilaya ni za muhimu kwa kuzingatia kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Mvomero ni Wakulima wanaotegemea Kilimo na shughuli za biashara ndogondogo. Hata hivyo, ustawi wa vyama vya kilimo/Mazao bado sio wa kuridhisha japokuwa uanzishaji wa vikundi vya uzalishaji umekuwa ukijitokeza katika baadhi ya maeneo.
Pamoja na mikakati ya kuhakikisha Ushirika unawanufaisha Wananchi, huduma hii kwa sasa inatolewa na vyama 22. Vyama 17 vikiwa ni vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, chama kimoja (1) kikiwa kinajishughulisha na Kilimo cha Mbogamboga na kuuza Pembejeo Mgeta. Chama kimoja (1) kinajishughulisha na Kilimo cha umwagiliaji Dakawa. Vyama viwili ambavyo ni Laramatak cha Kambala ni chama cha Ushirika wa wafugaji na Turiani AMCOS ambacho ni chama Ushirika cha Kilimo. Hivi ni vyama ambavyo tayari vimesajiliwa.
Vilevile kuna vyama 2 vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kutoka Maskati na Melela viko kwenye mchakato wa kusajiliwa na kimoja cha ufugaji wa Mbuzi wa Maziwa kutoka Mgeta nacho kiko katika mchakato wa kusajiliwa.
Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo
Wilaya ina jumla ya vyama vya Akiba na Mikopo 17 ambavyo vina jumla ya wanachama 6726, Me 4597, Ke 2129 vikiwa na Hisa 435,091,000/=, Akiba 473,790,000/= na Amana 411,622,000/=. Pia vimeweza kutoa Mikopo yenye thamani ya Tshs. 5,177,457,000/= ."Hali Halisi angalia Jedwali A"
Mbali na kuwa na SACCOS 17, Wilaya ina Vyama 5 (vitano) vya Ushirika ambavyo vinajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, maduka, umwagiliaji, kilimo cha nafaka na ufugaji. Vyama hivi vina jumla ya wanachama 961, Me 760 na Ke 201. Pia vina Hisa zenye thamani ya Tshs. 9,542,000/=
|
|
Na | Aina Ya Chama | Idadi Ya Wanachama | Jumla |
Me | Ke | Vikundi |
1 | SACCOS | 2,708 | 1,381 | 142 | 4,231 |
2 | Mazao | 127 | 20 | - | 147 |
3 | Shughuli Maalum | 27 | - | - | 27 |
Jumla | 2,885 | 1,401 | 142 | 4,398 |
|
|
Elimu |
|
Wilaya Mvomero ina jumla ya shule za msingi 139, kata za kielimu 18, shule za Sekondari 24. Kati ya hizo, shule 21 ni za wananchi, shule 1 ya Mzumbe ni ya Serikali Kuu na shule 2 ni za binafsi ambazo ni Askofu Adrian Mkoba inayoongozwa na dhehebu la Roman na Dr. Mezger chini ya Tanzania Youth Ministries (TAYOMI). Aidha kuna Chuo Kikuu kimoja cha Mzumbe na chuo cha ualimu Mhonda kinachotoa mafunzo ya ualimu kwa walimu wa daraja la III A.
|
|
Elimu ya Awali
|
|
Katika shule za msingi 139 zilizopo, shule 95 sawa na 68% zina madarasa ya awali. Shule hizo zina jumla ya wanafunzi 471 0wakiwemo wavulana 2347 na wasichana 2336. Aidha shule 44sawa na 32% hazina madarasa ya awali. Mkakati wa Halmashauri ni kuhakikisha kuwa kila shule ya msingi inakuwa na darasa la awali ifikapo 2010.
Walimu wanaofundisha Elimu ya awali ni miongoni mwa wanaofundisha shule za msingi ambao idadi yao ni 103, kati yao wanaume ni 35 na wanawake ni 68.
Mahitaji ya walimu kwa Elimu ya awali ni 196, waliopo ni 103, hivyo uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ni 1:47 (kiwilaya) na 1:25 (Kitaifa) kwa mantiki hiyo, Wilaya ina upungufu wa walimu wa awali 93.
|
|
Elimu ya Msingi
|
Halmashauri ya Wilaya ina jumla ya wanafunzi 62,627 wakiwemo wavulana 31,650 na wasichana 30,977. Walimu waliopo ni 1,434 kati yao wanaume ni 638 na wanawake ni 796. Mahitaji ya walimu ni 1,566 hivyo tuna upungufu wa walimu 132. Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kiwilaya ni 1:44 na kitaifa ni 1:40.
Uandikishaji darasa la I, 2008
Halmashauri ilitegemea kuandikisha watoto 8,489 kwa mwaka 2008, kati yao wavulana ni 4,240 na wasichana 4,249. Walioandikishwa ni 9,244 (wavulana 4,694, wasichana 4,550) sawa na asilimia 108.9%. Uandikishaji kwa miaka mitatu mfululizo umekuwa ukiongezeka kama inavyooneshwa katika jedwali Na. 1 hapo chini. Ongezeko hilo linatokana na uhamasishaji kwa wazazi kuwaanzisha shule watoto wote wenye umri wa miaka saba. Aidha ongezeko limechangiwa na mwamko wa elimu kwa jamii ya wafugaji kuwapeleka watoto wao shule.
|
|
Elimu ya Sekondari
|
|
Halmashauri ya Wilaya ina jumla ya shule za Sekondari 24. Kati ya hizo, shule 21 ni za wananchi, 1 ya Serikali Kuu na shule 2 za binafsi. Aidha kila kata ina shule ya Sekondari ya Kata na baadhi ya kata zina shule zaidi ya moja. Kata zenye shule zaidi ya moja ni Mtibwa (2), Diongoya (2), Mzumbe (2) na Mvomero (2). Idadi ya wanafunzi wote kuanzia kidato cha I – IV ni 7158, wakiwemo wavulana 4084 na wasichana 3074. Shule zenye kidato cha V - VI ni Askofu Adrian Mkoba na Mzumbe zenye jumla ya Wanafunzi 396 wakiwemo Wavulana 291na Wasichana 105.
Changamoto
Halmashauri bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu kwa shule za sekondari. Mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari kwa mwaka 2008, ni walimu 542, waliopo ni walimu 281 na upungufu ni walimu 261. Hata hivyo wapo walimu wa ajira mpya wapatao 15 wa “A” Level waliopangwa wilaya ya Mvomero, wanatarajiwa kuripoti ili kupunguza upungufu uliopo.
|
|
Maji |
Upatikanaji wa huduma ya maji
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 ina idadi ya watu 260,525. Idadi ya watu wanaopata maji safi na salama katima umbali usiozidi M. 400 imefikia 135,473 ambao ni sawa na asilimia 52 hadi kufikia mwaka wa fedha 2007/2008. Idadi ya wananchi wasiopata maji safi na salama ni 125052.
Miundo mbinu ya huduma ya maji
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ina miundombinu 328 na vituo 607 vinayotoa huduma ya maji kwa wakazi wake. Kati ya vituo hivyo, 444 ndivyo vinavyofanya kazi sawa na 73% ya vituo vyote kama ilivyooneshwa katika majedwali hapo chini:-
: Idadi na aina ya muradi ya maji
Na | Aina ya Miradi | Idadi |
1 | Miradi ya maji mtiririko/mserereko |
22
|
2 | Miradi ya maji ya kusukuma kwa mashine |
7
|
3 | Mabwawa/Malambo |
6
|
4 | Visima virefu |
17
|
5 | Visima vifupi |
274
|
6 | Uvunaji maji ya mvua |
2
|
JUMLA |
328
|
|
|
Changamoto |
Kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa kushirikiana na Wizara ya maji.
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's), Makampuni binafsi na ya Kiserikali, Taasisi za Kiserikali (DDCA) na zisizo za Kiserikali pamoja na wadau mbalimbali.
Kuendelea kutafuta na kuvutia wafadhili katika miradi ya maji ili tuweze kuboresha na kuifanyia matengenezo miradi iliyoharibika hasa ya mserereko ambayo inatoa matokeo haraka na inaweza kuhudumia vijiji zaidi ya kimoja.(Quick wins )
Kuendesha miradi ya maji ya jamii kwa kutumia jumuia za watumiaji maji. (WUA) zilizosajiliwa kisheria au mawakala.
Halmashauri kupitia timu ya uhamasishaji masuala ya maji na usafi wa mazingira ya wilaya (DWSST) kwa kushirikiana na shirika la EEPCO pia WATSANET imeweza kuunda na kusajili jumuiya mbili (2) za watumia maji (WUA) kati ya 6 zilizohitajika. Hata hivyo jitihada za kukamilisha jumuiya zilizobaki zinaendelea pamoja na kuhamasisha vijiji vingine vinavyotumia kamati za maji kuweza kubadili mfumo wa uendeshaji.
Kuhakikisha kuwa vyombo vinavyoendesha miradi ya maji jamii vinapatiwa mafunzo juu ya usimamizi na uendeshaji ili miradi hiyo iwe endelevu.
Kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na usafi wa mazingira.
Kutoa elimu kwa jamii juu ya utaratibu na kanuni za uchimbaji visima ili kudhibiti uchimbaji holela, pia kudhibiti matumizi ya maji kwa kuwapatia Water right wale wanaovuna maji zaidi ya kiwango kilichowekwa na Wizara.
|
|
Mifugo |
Shughuli zinazotekelezwa katika kuboresha maendeleo ya mifugo ni:-
Kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mbinu za ufugaji bora na uboreshaji mifugo
Kutoa tiba na kinga kwa magonjwa ya milipuko.
Kufanya ukaguzi wa nyama na ngozi
Kudhibiti magonjwa ya kupe na ndorobo
Kuendeleza nyanda za malisho kwa kuboresha majosho na malambo
Kusimamia minada na kukusanya mapato ya Halmashauri
Kutoa mafunzo kwa wafugaji 13 juu ufugaji wa kiabiashara
Kutoa mafunzo kwa wafugaji 135 juu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani
(i). Idadi Mifugo
Wilaya ya Mvomero ina jumla ya wafugaji ni 2,534 ambao wanamiliki mifugo kama ifuatavyo: Ngo'mbe wa kienyeji 172,827, ng'ombe wa maziwa 3,385, Mbuzi 51,161, Kondoo 20,121, Punda 385, Nguruwe 6,243, Kuku wa kienyeji 167,038, Kuku wa mayai 1,674, kuku wa nyama 6,946, Bata 12,018, Bata mzinga 35, Kanga 811, sungura 3,803, Mbwa 4,480.
(ii). Utengaji wa maeneo ya Ufugaji
Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji kwa njia ya kuandaa mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi ni 14. Vijiji hivi ni kati ya vijiji 22 vilivyotambuliwa kuwa na maeneo ya Wafugaji katika Wilaya.
Migogoro ya Wakulima na Wafugaji
Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Kambala:
Mgogoro kati ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Kambala kata ya Hembeti tarafa ya Turiani ni sugu hadi sasa uko mahakama kuu kitengo cha ardhi. Huu mgogoro unatokana na serikali ya kijiji cha Kambala ambacho wakazi wengi ni wafugaji kutotambuliwa na wakulima kutoka manispaa ya Morogoro ambao walipewa maeneo ya kulima mpunga katika bonde la mto Mgongola na uongozi wa mkoa miaka ya 1980 wakati wa Operesheni Nguvukazi. Wakulima wamekuwa wakizuiwa kulima katika hayo maeneo kwa sababu tayari eneo limetengwa kwa ajili ya ufugaji, lakini wakulima hao wanadai eneo ni la kilimo. Mgogoro huu uko Mahakamani.
Hali ya mifugo kiafya ni nzuri. Malisho na maji yanapatikana japo yamepungua kwa kipindi hiki. |
|
|
Viwanda, Biashara na Masoko |
• Hali ya Viwanda/Viwanda Vidogo vidogo
Wilaya ya Mvomero ina Kiwanda kikubwa 1 cha Mtibwa kinachozalisha Sukari (Mtibwa Sugar Estate) kilichopo kijiji cha Lukenge kata ya Mtibwa Tarafa ya Turiani. Kiwanda hiki kinamilikiwa na Mwekezaji Super Doll wa Dar es Salaam. Wilaya pia ina Kiwanda cha kati, ambacho. ni Kiwanda cha kusindika nyama ya ng'ombe na kuku kilichopo kijiji cha Nguru ya Ndege. Kiwanda kina mpango wa kupunguza kukidhi soko la ndani na pia kuuza nyama iliyosindikwa nje ya nchi. Lengo la mradi huu ni kuchinja ng'ombe 300 kwa siku utakapokamilika.
Vipo viwanda vidogo vya useremala, mashine za kukamua mafuta, mashine za kusaga n.k. pia kuna Kiwanda kimoja cha kusindika sukari guru kilichopo kata ya Mlali.
(ii). Matumizi ya Vipimo halali kwa mujibu wa sheria ya vipimo Na. 20 ya 1982 na marekebisho yake katika kuzingatia matumizi ya vipimo halali kwa mujibu wa sheria ya vipimo na 20 ya 1982 na marekebisho yake. Idara kwa Kushirikiana na Wakala wa vipimo mkoani ilifanya ukaguzi wa mizani.
AFYA |
Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni mojawapo ya Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
(i). Hali ya Afya
Hali ya afya na chanjo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imeanishwa katika jedwali hapo chini:- |
VIASHIRIA MUHIMU | KIWANGO |
2005 | 2006 | 2007 |
Vifo vya Watoto Wachanga | 88/1000* | 99/1000* | 68/1000* |
Vifo vya Watoto chini ya Miaka mitano | 188/1000 | 112/1000 | 90/1000 |
Vifo vya Uzazi | 748/100,000 | 478/100,000 | 457/100,000 |
Kiwango cha Wazazi wanaozalishwa na Wakunga waliopata mafunzo | 55 % |
68 % |
72% |
Kiwango cha Maambukizi ya VVU/UKIMWI | 8.5% | 6.2% | 4.5% |
|
|
MMAM
|
Lengo kuu la Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ni kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi. Katika Wilaya ya Mvomero kama ilivyo kwenye Wilaya nyingine hapa Tanzania idadi kubwa ya watu wanaishi zaidi ya kilomita tano kutoka kituo cha kutolea huduma ya Afya. Kwa Mama Mjamzito kutembea kilometa tano kwenda kupata huduma na kurudi ni umbali mkubwa na zaidi ya hayo vituo vingine vya huduma havifikiki kutokana na kuwapo mito, mabonde au milima. MMAM inakusudiwa kwamba kila kijiji kiwe na zahanati na kila Kata iwe na Kituo cha Afya pia kila Wilaya iwe na Hospitali ya Wilaya ili kila mtu aweze kuwa jirani zaidi na kituo cha kutolea huduma za Afya kinachofikika kwa urahisi. Wilaya ya Mvomero ina jumla ya Vijiji 101 kati ya hivyo Vijiji vyenye zahanati angalau moja au zaidi ni Vijiji 59 na ambavyo havina zahanati ni 43.
|
|
|
Vitendea kazi |
|
Usafiri :
Idara ya Afya ina jumla ya magari sita (6).
• Magari ya Vituo vya Afya (Ambulance) kwa ajili ya kusafirisha Wagonjwa ni 3,
• Gari la usimamizi wa huduma za Afya na usambazaji wa Chanjo 1,
• Usimamizi wa huduma za Afya, Usambazaji na Utawala 1 na
• Gari la mizigo(Lori) kwa ajili ya kusafirishia vifaa tiba na vifaa vya ukarabati 1.
Idadi ya pikipiki ni 11 , kati ya hizo 6 ni za Wasimamizi wa huduma za Afya ngazi ya Kanda (CASCADE) na 5 za Miradi mbalimbali ya huduma za Afya (Usubi, Chanjo, UKIMWI).
Dawa :
Wilaya Mvomero ipo katika mfumo wa kuagiza dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya madawa (MSD) kutokana na mahitaji ya Kituo cha kutolea huduma (Indent) kila baada ya miezi mitatu, mara dawa zikifikishwa makao makuu ya Wilaya husambazwa katika zahanati zote na Vituo vya
|
|
|
Changamoto |
Changamoto zinazoikabili Sekta ya Afya ni pamoja na:
Upungufu wa Watumishi wenye ujuzi ukilinganisha na vituo vilivyopo na vipya vinavyojengwa.
Upungufu wa vitendea kazi vya kitaalamu na vya kawaida.
Upungufu wa nyenzo za usafiri ukilinganisha na majukumu ya Idara kama vile ukosefu wa gari la usamabazaji la kujitegemea kama miongozo inavyoelekeza.
Upungufu wa madawa toka Bohari la madawa (MSD) yanapoagizwa.
Ukosefu wa miundombinu bora kama barabara inayokwamisha kupeleka vifaa, tiba na vya ujenzi pamoja na madawa kwa wakati hususani kipindi cha mvua.
Majengo yaliyochakaa katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Wagonjwa wa UKIMWI/VVU kusafiri mwendo mrefu kufuata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs).
|
|
Barabara |
Hali ya barabara kwa kilometa Wilaya ya Mvomero ina mtandao wa barabara zenye jumla ya urefu wa km. 831.47 ambazo zinagawanyika katika makundi makuu manne:-
Barabara Kuu km. 112.08 Barabara za Mkoa km. 232.89 Barabara za Wilaya km. 79.60 Barabara za Vijiji km. 406.90
Barabara kuu na za Mkoa zinazopitika ndani ya Wilaya ya Mvomero zinahudumiwa na Wakala wa barabara wa Mkoa wa Morogoro (TANROADS) na barabara za Wilaya na za Vijiji zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Matengenezo/ukarabati wa barabara Mpango kazi wa Matengenezo ya Barabara Mwaka Wa Fedha 2008/2009.
Wilaya ya Mvomero inahudumia barabara zake kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo Mfuko wa Barabara (Roads Fund), Mradi wa Usafiri na Uchukuzi Vijijini (VTTP) na Mpango wa Maendeleo ya barabara vijijini (LGTP).
Aina za matengenezo Halmashauri inahudumia barabara zake kwa kuzifanyia matengenezo yafuatayo:-
Matengenezo ya kawaida ( Routine Maintenance)
Matengenezo ya sehemu korofi (Spot Improvement)
Matengenezo ya muda maalum (Periodic Maintenance)
Matengenezo ya Madaraja na Makalvati (Bridges and culverts)
Katika mwaka wa fedha 2008/2009 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imejipangia kufanya matengenezo ya barabara zake kwa kutumia fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa jumla ya Tshs. 668,300,000/= kama ifuatavyo:-
Mfuko wa Barabara (Roads Fund) Matengenezo ya kawaida km. 206.4 Tshs. 144,700,000.00 Matengenezo ya sehemu korofi km. 32 Tshs. 40,000,000.00 Matengenezo ya muda maalum km 19 Tshs. 192,000,000.00 Matengenezo ya Madaraja na Makalvati Tshs. 20,000,000.00 Usimamizi wa matengenezo Tshs. 24,600,000.00 JUMLA Tshs. 421,300,000.00
|
|
|
Hifadhi ya Mazingira |
Hali ya utunzaji mazingira na uzingatiaji wa sheria ya mazingira ya 2003
Halmashauri imekuwa inatekeleza majukumu yake kufuatana na sera ya misitu ya 1998 na sheria ya misitu ya 2002, na ya wanyamapori ya 1998 “Ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na kuzingatia matumizi endelevu”.
Halmashauri pia imekuwa ikitekeleza sera na sheria ya Mazingira ya 1997 na 2004 ” kuhusu Uzingatiaji wa athari za kimazingira popote tulipo”.
Halmashauri inatoa elimu kwa wananchi juu ya miti ya Misederela na kutunga sheria ndogo za udhibiti upandaji wa miti hiyo jirani na misitu ya hifadhi. Vijiji 44 vya kata za Melela, Doma, Tchenzema, Mvomero, Turian na Hembeti vimepatiwa mafunzo ya hifadhi ya mazingira, kati ya vijiji 101 vya wilaya ya Mvomero.
Elimu ya Mazingira na athari za uchomaji moto misitu ilitolewa. kwa kipindi cha Julai hadi Juni 2007/2008, Halmashauri ilitumia gari la wizara Mobile video van kutoa elimu na kuonesha picha za video katika vijiji 8 vilivyo chini ya mpango wa usimamizi shirkishi wa misitu (USM) na katika vijiji vya Melela, Mlandizi na Nyandira. Katika utoaji wa mafunzo hayo mwitikio umekuwa mkubwa na mabadiliko yamekuwa makubwa kwani athari za mazingira zimepungua.
|
|
Mikakati |
Halmashauri imefanya doria za mara kwa mara katika barabara kuu za Iringa na Dodoma kwa ajili ya udhibiti wa mkaa. Hata hivyo jamii kwenye vijiji wamefundishwa sheria ya Misitu ya 2002 na kisha kuunda kamati za udhibiti wa uharibifu wa mazingira za vijiji.
Sheria ndogo za kuhifadhi misitu, na kudhibiti uchomaji wa moto zimeundwa katika vijiji vya Tchenzema, Nyandira, Kibuko, Mwarazi, Kanga, Dihinda, Mziha na Difinga. Mchakato wa kutunga sheria ndogo za kudhibiti uchomaji moto misitu katika vijiji nane vya mpango wa usimamizi shirikishi unaendelea.
Katika kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vya Manza, Wami Dakawa, Makuyu, na Tangeni wananchi wameainisha njia za kudhibiti uchomaji moto ikiwa ni pamoja na kuandaa sheria ndogo. Katika maeneo yaliyotajwa sheria zimekamilika na zinatumika.
Kamati za Mazingira za vijiji (Village environmental Management committees) zimeundwa ama kuimarishwa na kwa kushirikiana na Serikali za vijiji , zimesaidia katika kuwakataza watu kuvamia misitu na kwenda kuishi au kuanzisha mashamba bila idhini ya serikali ya kijiji husika. Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti matukio ya moto yanayotokana na uaandaji wa mashamba au malisho ya mifugo.
Katika kipindi cha 2007/2008 kamati za mazingira katika vijiji vya Tchenzema, Nyandira, Kibuko, Mwarazi Manza, Wami Dakawa, Makuyu, Nyandira, Tangeni, Mangae, Msongozi na Maharaka ziliundwa na kupatiwa Mafunzo.
|
|
Ardhi |
Wilaya ya Mvomero ni moja wapo kati ya Wilaya zilizogubikwa na migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro.Mingi ya migogoro ni ya zamani na imeshughulikiwa tangu enzi za Wilaya mama ya Morogoro Vijijii ikiwa ni pamoja na kuundiwa Tume za Kitaifa. Migogoro mikubwa kati ya migogoro mingi ya ardhi Wilayani ni pamoja na:
Mgogoro kati ya Kijiji cha Melela na Ushirika wa Twende Pamoja
Mgogoro katika kijiji cha Melela kati ya wakulima wa Ushirika wa Twendepamoja kutoka Manispaa ya Morogoro na wafugaji ni wa muda mrefu. Wakulima kutoka mjini Morogoro walivamia ardhi katika kitongoji cha Mela mwaka 1999 kilichotengwa na wanavijiji kwa ajili ya wafugaji. Huu mgogoro ulipelekwa mahakamani na Twende pamoja walishindwa kwenye kesi sasa wameungana na wanakijiji waliokuwa wanaishi Mela na wameishitaki Halmashauri, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Melela na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mela walipwe fidia ya Sh. bilioni 10 kwa ajili ya mashamba waliyonyang'anywa. Bado kesi ipo Mahakamani na hivi karibuni Waziri Mkuu ameunda tume ya kuchunguza mgogoro huo na bado hatujajua majibu ya Tume.
Mgogoro kati ya shamba la Kipunguni Enterprises Ltd na vijiji jirani:
Mgogoro mwingine ni kati ya Kipunguni Enterprises LTD mmiliki wa shamba lenye ukubwa wa karibia ekari 98,000 linaloenea katika vijiji vitano vya Mangae, Msongozi, Mkata, Melela na Magali. Mashamba na makazi ya wanavijiji yamo ndani ya hilo shamba ambalo hapo awali lilikuwa likimilikiwa na MODECO na baadae mwaka 1975 likauzwa kwa zabunikwa Kipunguni Enterprises Ltd. Uongozi wa wilaya una mpango wa kuwasiliana na mmiliki ili aachie kwa hiari maeneo yaliyokaliwa na wanavijiji ili iwe ardhi ya vijiji.
|
|
|
Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi
|
Mipango ya matumizi bora ya ardhi imeandaliwa katika vijiji 20 kati ya vijiji 101 vya Wilaya. Malengo ya mwaka 2008/2009 ni kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 11.
|
|
Utoaji hati na vyeti vya ardhi |
Vijiji vyote 101 vimepimwa mipaka kwa ufadhili wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ramani zimekamilika hivi karibuni. Hatua inayofuata ni kutayarisha vyeti vya ardhi ya Vijiji kwa kuanza na vijiji 20 ambavyo tayari vimeandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Baada ya hapo vijiji vitapewa cheti cha ardhi ili Ofisi za vijiji zianze kutoa hati za hakimiliki za kimila kwa eneo la kila mwanakijiji. Wanakijiji watazitumia hati hizo kama dhamana ya upatikanaji wa mikopo .
|
|
Upimaji mashamba |
Upimaji wa ranchi 50 za wafugaji eneo la Dakawa umeshaanza lakini bado haujakamilika kutoka na ugumu wa upatikanaji wa vifaa vya upimaji.
Utoaji hatimiliki za mashamba
Utoaji wa hatimiliki za mashamba utafanyika baada ya kazi ya upimaji ranchi 50 kukamilika.
Utwaaji wa mashamba yasiyoendelezwa
Mashamba 34 yamewasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kubatilisha hatimiliki ambayo ni kati ya mashamba 68 yenye ukubwa wa hekta 54,193 yaliyotambuliwa kuwa hayaendelezwi.
Ufugaji nyuki
Katika kipindi cha 2007/2008 Halmashauri, watu binafsi na mashirika yasiyo ya Kiserikali imevuka lengo la kutundika mizinga 500 ambapo mizinga 629 imetundikwa sehemu mbalimbali na mingi ya hiyo ina asali. Bado utaratibu unaendelea wa kusimamia zoezi hilo ili liwe la manufaa kwa jamii kama njia ya kuinua kipato. Sekta inafanya utaratibu wa kupata soko la uhakika hapa mkoani Morogoro na Dar es Salaam. |
|
We need information on villages.
ReplyDeleteTujitahidi kuimarisha mawasiliano ya barabara kutoka Kara moja na nyingine ili kurahisisha utoaji wa huduma na mawasiliano
ReplyDeleteVp mbona cjaona vyanzo vya maji au hamna kabisa katika wilaya ya mvomero?
ReplyDelete